WAMILIKI WA VITUO VYA WATOTO YATIMA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA

TAREHE 28-11-2017


Wamiliki wanaoendesha vituo vya kuwalea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu hapa nchini wametakiwa kufuata sheria za uanzishwaji wa vituo hivyo ikiwemo kuvisajili na kutoa huduma bora kwa watoto hao.

Kauli hiyo imetolewa na afisa ustawi wa jamii kutoka halmashauri ya Meru Bi Restuta Mvungi wakati akizungumza na Redio Safina kuhusu huduma  zinazotakiwa kutolewa katika vituo mbalimbali vinavyotunza watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Bi Mvungi amesema kuwa baadhi ya huduma zinazotakiwa kutolewa na vituo hivyo ni pamoja na kuwa na nyumba nzuri,matibabu,malazi pamoja na lishe bora,na vituo ambavyo vinakiuka taratibu hizo vinachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuvifungia.

Amesema kuwa katika halmashauri ya Meru kuna vituo 30 na wao kama watu wa ustawi wa jamii wamekuwa wakitoa elimu kwa vituo hivyo ili wajue wajibu wao katika kuwahudumia watoto hao kama sheria ya mtoto inavyoelekeza.


Hata hivyo afisa huyo amewaonya wale wote wanaotumia vituo vya kuwalea watoto yatima kujinufaisha wenyewe na watakaobainika watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
WAMILIKI WA VITUO VYA WATOTO YATIMA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA WAMILIKI WA VITUO VYA WATOTO YATIMA WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA Reviewed by safina radio on November 28, 2017 Rating: 5

No comments