RAIS MAGUFULI AVIAGIZA VYOMBO VYA DOLA KUWACHUKULIA HATUA WATU WANAOTOA TAKWIMU ZA UONGO.
TAREHE 20-12-2017
Rais wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania Mh John Magufuli ameviagiza vyombo vya dola hapa nchini
kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote wanaotoa takwimu za uongo hapa
nchini na kupotosha jamii kuhusu maendeleo ya nchi.
Mh Magufuli ametoa
maagizo hayo leo muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi katika jengo la
takwimu ya taifa lililopo mkoani Dodoma,ambapo amesema kuwa kulingana na
kifungu namba 37 cha sheria za takwimu hapa nchini mtu anayetoa takwimu za
uongo adhabu yake ni kifungo cha miezi sita hadi miaka mitatu au faini ya
shilingi milioni kumi au adhabu zote kwa pamoja.
Amesema kuwa baadhi
ya watu wamekuwa wakitoa takwimu za uongo kuhusu ukuaji wa uchumi kwa lengo la
kukwamisha juhudi za serikali za kuwaletea wananchi wake maendeleo,hivyo
kuanzia sasa mtu yeyote atakayebainika kutoa takwimu za uongo atashughulikiwa
kwa mujibu wa sheria ya mwaka wa 2015.
Aidha Mh Magufuli
ameongeza kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu takwimu zinaonesha kuwa
uchumi wa Tanzania unaendelea kukua kwa asilimia 6.8 na kufanya Tanzania
kuongoza katika nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki na pia ni miongoni mwa nchi
tano barani Afrika ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi.
Kwa upande wake
mkurugenzi mkuu wa ofisi ya taifa ya takwimu Dr Albina Chuwa amesema kuwa ofisi
hiyo imekuwa ikifanya vizuri kimataifa,ambapo barani Afrika Tanzania imekuwa
nchi ya pili katika kutoa takwimu bora ikitanguliwa na nchi ya Afrika Kusini
kati ya nchi 54 za Afrika.
RAIS MAGUFULI AVIAGIZA VYOMBO VYA DOLA KUWACHUKULIA HATUA WATU WANAOTOA TAKWIMU ZA UONGO.
Reviewed by safina radio
on
December 20, 2017
Rating:

No comments