VIJANA NCHINI TANZANIA WASHAURIWA KUTUMIA FURSA WALIZONAZO
Vijana wameshauriwa kutumia furusa walizonazo ili
kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa kiongozi, si kuongoza
taasisi au kikundi fulani cha watu pekee bali hata kujiongoza mwenyewe ni
uongozi.
Ushauri huo umetolewa na mkurugenzi wa taasisi
isiyokuwa ya kiserikali ya LEAD Tanzania inayotoa mafunzo ya uongozi na jinsi
ya kujikwamua kiuchumi kwa vijana Bw.Nickson Kataze katika kongamano la uongozi
ambalo limefanyika katika kanisa la K.K.K.T Kimandolu mkoani Arusha.
Bw.Kataze amesema kuwa kijana anapaswa kutumia fursa
aliyonayo kujikwamua kiuchumi sambamba na kutambua kuwa yeye ni kiongozi wa
maisha yake ambapo taasisi ya LEAD Tanzania imejikita katika kuwawezesha vijana
katika maeneo ya elimu, mafunzo ya uongozi,na kuwawezesha kiuchumi.
Aidha ameongeza kuwa shirika hilo tofauti na mashirika mengine walianza kwa kufanya utafiti juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana ambapo walienda katika kata 5 na kuwahoji zaidi ya vijana elfu moja ambapo ripoti ya utafiti huo tayari imewasilishwa kwa mkuu wa wilaya na watendaji wa kata hizo.
Pia katika kongamano hilo vijana mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya mkoa wa Arusha walitoa shuhuda jinsi ambavyo mafunzo waliyoyapata katika taasisi hiyo yalivyowasaidia kujikwamua kiuchumi kwa kuweza kuanzisha vitega uchumi ambavyo awali kabla ya kupata mafunzo hayo walikuwa hawana.
Kwa upande wake afisa maendeleo wa jiji la Arusha Bw.
Polycap Nguyumba ameitaka taasisi hiyo kuendelea kutoa mafunzo ya uongozi kwa
watu mbalimbali yatakayo wasaidia kutoka sehemu moja hadi nyingine na kuongeza
kuwa maadili ni msingi wa uongozi.
Hata hivyo taasisi hiyo ya LEAD Tanzania yenye makao yake katika kanisa la K.K.K.T kimandolu ilianza
kazi rasmi mwezi machi mwaka jana ambapo kufikia sasa imefanikiwa kutoa mafunzo
ya uongozi kwa zaidi ya watu mia tano na inatarajia kuendelea kutoa mafunzo zaidi na hutolewa bure kwa yeyote anayeitaji.
VIJANA NCHINI TANZANIA WASHAURIWA KUTUMIA FURSA WALIZONAZO
Reviewed by safina radio
on
December 11, 2017
Rating:
No comments