WATANZANIA WASHAURIWA KUTUMIA SEHEMU YA MAPATO YAO KUSAIDIA YATIMA NA WASIOJIWEZA.

TAREHE 27-12-2017

Watanzania wametakiwa kujijengea tabia ya kutumia sehemu ya mapato yao kwa ajili ya kuwasaidia watoto yatima na watu wasiojiweza katika jamii ili kuwawezesha kujikwamua na umasikini na kufikia ndoto zao.

Hayo yamesemwa na operation  meneja wa kampuni  inayojihusisha na utalii wa kitamaduni ya Tengeru cultural tourism Bw. Ruben Samweli Palangyo wakati akikabidhi msaada wa vyakula na vinywaji kwa watoto yatima katika vituo vya yatima vya Global na Ikunda vilivyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Bw. Pallangyo amesema kuwa kampuni hiyo imejiwekea utaratibu wa kutumia sehemu ya mapato yake kusaidia yatima na watu wasiojiweza katika jamii kwani hawajapenda kuishi maisha waliyonayo hivyo ni vyema makampuni mengine na watu binafsi kutenga sehemu ya mapato yao kuwasaidia.

Kwa upande wake mratibu wa Tengeru cultural tourism Bi. Sara Gadi amesema kuwa wameguswa na uhitaji wa watoto yatima ndio maana wamejiwekea utaratibu wa kutumia sehemu ya pato lao kuwasaidia na kuitaka jamii kuungana kwa pamoja kuwasaidia yatima na watu wasiojiweza katika jamii.

Bi. Sara ameongeza kuwa ni vyema jamii nzima ikaungana kwa pamoja kuwasaidia yatima kwani  hawakupenda kupoteza wazazi wao na bado wana ndoto kubwa katika maisha yao kama walivyo watoto wenye wazazi na wakuwasaidia ni jamii.

Naye mlezi wa kituo cha Ikunda Mchungaji Betrice Izrael Kishe amesema kuwa kazi ya kulea yatima ni wito kutoka kwa Mungu hivyo wenye vituo hawapaswi kuzunguka kuomba misaada kwani mwenye kituo ni Mungu na atawatumia watu kupeleka misaada.


Aidha Bw. Macdonald Elifasi Kaaya mlezi wa watoto katika kituo cha Global  ameishukuru kampuni ya Tengeru cultural tourism kwa msaada walioutoa na kuwataka watu mbalimbali kutumia njia ya kusaidia yatima kuteka baraka lakini pia kama njia ya kumtumikia Mungu.

Hata hivyo Zakaria Simon kutoka kituo cha global orphanage kwa niaba ya wenzake ameishukuru kampuni hiyo kwa kuwambuka.
WATANZANIA WASHAURIWA KUTUMIA SEHEMU YA MAPATO YAO KUSAIDIA YATIMA NA WASIOJIWEZA. WATANZANIA WASHAURIWA KUTUMIA SEHEMU YA MAPATO YAO KUSAIDIA YATIMA NA WASIOJIWEZA. Reviewed by safina radio on December 27, 2017 Rating: 5

No comments