Taarifa ya habari 13 sept 2017 saa 7:00 mchana

DODOMA.
Waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Mh Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali imeongeza vituo 150 kwa ajili ya kutoa huduma za uzazi wa dharura ili kuokoa vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi.

Mh Mwalimu ameyasema hayo katika kikao cha wabunge wa klabu ya uzazi salama,ambapo amesema kuwa katika kufanikisha suala hilo serikali imeandaa fedha kwa ajili ya kujenga vituo vitano vya kuhifadhia damu salama kwa ajili ya upasuaji wa wanawake wanapojifungua.

Amesema kuwa serikali pia imeongeza bajeti ya uzazi salama kutoka bilioni 16 hadi bilioni 32,ambapo kwa sasa ni vituo vya afya vya serikali mia moja ishirini tu vinavyotoa huduma ya uzazi wa dharura hivyo serikali ameamua kuongeza vituo vingine mia moja hamsini ili vifikie mia mbili tisini kati ya mia tano hamsini na sita vinavyotakiwa.

Hata hivyo takwimu zinaonyesha kuwa,katika kila wanawake laki moja hapa nchini wanawake mia tano hamsini na sita wanaojifungua hupoteza maisha kila mwaka kutokana na uzazi.



.........................................................................................................................
ARUSHA.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw Mrisho Gambo amemwagiza mkurugenzi wa halamashauri ya Arusha na katibu tawala wake kutafuta ufumbuzi wa tatizo la wananchi kutozwa fedha kwa ajili ya kupimiwa ardhi ili waweze kupewa hati za kimila.



Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw Mrisho Gambo 


























Bw Gambo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa kitongoji Ingorora na pasiliani kata ya Kisongo katika halmashauri ya Arusha akiwa katika ziara ya siku tano yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi,ambapo amesema kuwa ni lazima majibu sahihi yatolewe ili kuweza kufahamu undani wa suala hilo.

Amesema kuwa haiwezekani jambo lifanywe na serikali wananchi wachangishwe fedha na jambo hilo lisieleweke hivyo mkurugenzi pamoja na katibu wanatakiwa kufuatilia tatizo hilo na kisha kuwasilisha majibu yake kwake kwa njia ya maandishi na ameahidi kurudi tena katika kata hiyo kufuatilia majibu ya maagizo aliyoyatoa.

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Arusha yupo katika ziara ya siku tano katika halmashauri ya Arusha ikiwa ni utaratibu wake aliojiwekea ya kutembelea wilaya na halmashauri zote za mkoa wa Arusha lengo likiwa ni kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.



.......................................................................................................................... 


DODOMA.
Naibu waziri wa fedha na mipango Dr Ashantu Kijaji amesema kuwa lengo la serikali kuamua kukusanya kodi za majengo katika halmashauri na majiji hapa nchini ni ili kuongeza mapato mengi zaidi yatakayosaidia kuwaletea wananchi wa hali ya chini maendeleo.

DR Ashantu Kijaji.





Dr Kijaji ameyaseama hayo leo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu Mh Cecilia Pareso aliyetaka kujua serikali kuu imefanikiwa kukusanya kiasi gani cha fedha kuanzia ilipoanza kukusanya kodi za majengo katika halmashauri na majiji hapa nchini.

Amesema kuwa ili kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi ni lazima serikali ipate mapato ya kutosha,ambapo katika mwaka wa fedha wa 2015/16 na 2016/17 mamlaka ya mapato Tanzania imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 34 katika halmashauri,manspaa na majiji 30 hapa nchini tofauti na hapa awali ambapo ukusanyaji ulikuwa ni shilingi bilioni 28 pekee.

Ameongeza kuwa,fdha zinazopatikana katika makusanyo hayo zinapelekwa katika halmashauri ili ziweze kutatua kero za wananchi kama ilivyo azma ya serikali ya awamu ya tano kuwahudumia wananchi wa hali ya chini ili waweze kuondokana na umaskini na kufikikia uchumi wa kati ifikapo mwaka wa 2025.

Hata hivyo bunge la kumi na moja mkutano wa nane unaendelea mjini Dodoma,ambapo pamoja na mambo mengine wabunge watajadili na kupitisha miswada mitatu ya sheria na bunge hilo litahitimishwa Septemba 15 mwaka huu.
.............................................................................................................
                                        KIMATAIFA .
NAIROBI.
Polisi nchini Kenya wamewakamata watu wanne wanaoaminika kuwa raia wa Burundi ambao walikuwa wakielekea Somalia kujiunga na kundi la al-Shabab.

polisi nchini Kenya wakamata raia wa burundi 

Msemaji wa poli nchini Kenya George Kinoti amesema kuwa maafisa wa ujasusi walikuwa wakiwafuata washukiwa hao baada ya kupata habari kuhusu mipango yao.
Ameongeza kwamba washukiwa wanne walikamatwa katika kizuizi cha polisi mjini Isiolo takriban kilomita mia tatu hamsini  kaskazini mwa mji mkuu wa Nairobi wakielekea katika mji wa mpakani wa Mandera.
Maafisa wa polisi pia wanasema wanne hao waliingia nchini Kenya kama watalii kupitia visa huru ya ushirikiano kati ya Burundi na Kenya.
Maafisa katika Ubalozi wa Burundi mjini Nairoibi wanasema kuwa watatoa taarifa kamili kuhusu kukamatwa huko baada ya kushauriana na mamlaka ya Kenya.


...................................................................................................................................................................

PYONGYANG.
Korea Kaskazini imeapa leo kuuharakisha mpango wake wa silaha za nyuklia kama hatua ya kujibu vikwazo ilivyowekewa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa baada ya jaribio lake la sita na kubwa kabisa la silaha za nyuklia.
Wizara ya mambo ya nchi za kigeni ya Korea Kaskazini imesema katika taarifa kwamba taifa hilo litaongeza maradufu juhudi za kujiimarisha ili kuulinda uhuru na haki yake.
Vikwazo vipya vilivyoandaliwa na Marekani vilipitishwa siku ya Jumatatu na vinajumuisha marufuku ya kuuza nguo katika nchi za nje na kudhibiti usafirishaji wa bidhaa za mafuta kuuadhibu utawala wa Pyongyang kwa jaribio hilo.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema hatua kali zaidi zinahitajika kuchukuliwa dhidi ya Korea Kaskazini baada ya vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa.

 .........................................................................................................................


CARACAS.
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amesema yuko tayari kukutana na upinzani kwa mazungumzo yanayosimamiwa na Jamhuri ya Dominican na waziri mkuu wa zamani wa Uhispania Jose Luis Rodriguez Zapatero.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema serikali ya Venezuela itafanya awamu ya kwanza ya  mazungumzo katika Jamhuri ya Dominican leo.
Akizungumza baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Venezuela Jorge Arreaza mjini Paris, Le Drian amesema mazungumzo hayo yanasimamiwa na rais Danilo Medina wa Jamhuri ya Dominican na waziri mkuu wa zamani wa Uhispania Jose Luis Rodriguez Zapatero.
 Le Drian ameonya Venezuela huenda ikawekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya iwapo haitashiriki mazungumzo hayo,ambapo pua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anayaunga mkono kikamilifu mazungumzo hayo.


 Endelea kufuatilia ukurasa wetu kwa habari mbalimbali saa saba na saa mbili usiku. mshirikishe na mwenzako







Taarifa ya habari 13 sept 2017 saa 7:00 mchana Taarifa ya habari 13 sept 2017 saa 7:00 mchana Reviewed by safina radio on September 13, 2017 Rating: 5

No comments