WAFUGAJI WILAYANI BABATI MKOANI MANYARA WAHIMIZWA KUTUMIA MIFUGO WALIYONAYO KUBORESHA MAISHA YAO.

TAREHE 27-09-2017



Wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara wamehimizwa kutumia raslimali ya mifugo waliyonayo kuboresha maisha ya familia, kuwekeza katika elimu kwa  kuwapeleka watoto wao shule na kuchangia mipango ya maendeleo katika maeneo yao.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani humo Bw Raymond Mushi wakati akizindua zoezi la upigaji chapa ng’ombe katika kijiji cha Ngoley kata ya Mwada,ambapo amesema  kuwa idadi ya mifugo inayofugwa ni lazima  ilingane na eneo la malisho ili ufugaji uwe  wenye tija.

Amesema wafugaji wakitumia rasilimali walizonazo ambazo ni mifugo kwa tija wataweza kufuga kisasa na kuboresha maisha yao ambayo yatasaidia kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa ikiwa ni pamoja na kuinua uchumi wa mkoa huo.

Aidha amesema zoezi hilo la kupiga chapa Ngombe hao ni agizo la Serikali kupitia wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi la kuanza upya zoezi la kuweka alama ng’ombe ili kutimiza sheria ya utambuzi usajili na ufuatiliaji mifugo kifungu cha 5(1) cha sheria namba 12 ya mwaka 2010 inayoelekeza mifugo yote kufanyiwa Utambuzi,Usajili na Ufuatiliaji.

Bw Mushi ametaja  faida za zoezi la Utambuzi,Usajili na Ufuatiliaji mifugo kuwa ni kudhibiti magonjwa ya mifugo,wizi wa mifugo,kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji, kuhakikisha usalama wa chakula cha mifugo na kuboresha bidhaa zitokanazo na mifugo.


Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Bw Hamisi Malinga amesema kuwa tangu zoezi hilo kuanza Julai 2017 kwa kutoa elimu, uhamasishaji na uandaaji wa vifaa jumla ya Ng’ombe elfu nne mia saba na sabini  wamepigwa chapa.
WAFUGAJI WILAYANI BABATI MKOANI MANYARA WAHIMIZWA KUTUMIA MIFUGO WALIYONAYO KUBORESHA MAISHA YAO. WAFUGAJI   WILAYANI   BABATI  MKOANI   MANYARA  WAHIMIZWA  KUTUMIA  MIFUGO   WALIYONAYO   KUBORESHA   MAISHA   YAO. Reviewed by safina radio on September 27, 2017 Rating: 5

No comments