RAIS WA TANZANIA JOHN MAGUFULI AMESEMA SERIKALI ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA WAWEKEZAJI .
TAREHE 31-10-2017
Rais
wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mh John Magufuli amesema kuwa serikali
itaendelea kushirikiana na wawekezaji mbalimbali wanaowekeza katika sekta ya
viwanda ili kukuza uchumi wa nchi na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Mh
Magufuli ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua kiwanda cha kuzalisha bidhaa za
Plastiki cha Vicktoria kilichopo eneo la Igogo wilayani Nyamagana Mkoani
Mwanza,ambapo amesema kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kukuza uchumi
wake kupitia sekta ya viwanda hivyo itaendelea kushirikiana na wawekezaji hao
ili azma hiyo iweze kufanikiwa.
Amesema
kuwa kwa muda mrefu sekta ya viwanda hapa nchini imekuwa haifanyi vizuri
kutokana na makosa aliyotendeka kipindi cha nyuma na kwa kutambua hilo serikali
imeamua kurekebisha makosa hayo kwa kuanzisha viwanda vingi ambavyo vitasaidia
kuwaajiri vijana wengi pamoja na kuchangia uchumi wa Taifa.
Kwa
upande wake waziri wa viwanda,biashara na uwekezaji Mh Charles Mwiijage amesema
kuwa kiwanda hicho mbali na kusambaza bidhaa zake hapa nchini kinauza pia nje
ya nchi na kusaidia taifa kupata fedha za kigeni na pia kimesaidia kuwaajiri
wafanyakazi zaidi ya mia tano na kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Hata
hivyo rais Magufuli yuko katika ziara ya siku mbili mkoani Mwanza,ambapo mbali
na kuzindua kiwanda hicho cha plastiki amezindua pia kiwanda cha kutengenezea
dawa za binadamu cha Prience Phamacetical Limited kilichopo wilayani Nyamagana
mkoani humo.
RAIS WA TANZANIA JOHN MAGUFULI AMESEMA SERIKALI ITAENDELEA KUSHIRIKIANA NA WAWEKEZAJI .
Reviewed by safina radio
on
October 31, 2017
Rating:

No comments