MANDA AAGIZA KUKAMATWA KWA WAZAZI WANAODAIWA KUWAFUNDISHA WATOTO KUJAZA MAJIBU YA UONGO.


MTWARA.


Taarifa ya Habari 01:00 mchana, 15 February, 2018.

Mkuu wa Wilaya Evod Manda. 

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evod Manda ameagiza kukamatwa kwa wazazi wanaodaiwa kuwafundisha watoto kujaza majibu ya uongo katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa kuogopa gharama za kuwapeleka wanafunzi shule za sekondari.

Manda ametoa agizo hilo katika kikao cha wadau wa elimu wa halmashauri ya Nanyamba kufuatia shule zaidi ya tano kubainika kuwa baadhi ya wazazi wa wanafunzi wa shule hizo wamewafundisha watoto wao kujaza majibu ya uongo kwenye mitihani yao ya kumaliza darasa la saba ili wafeli katika mitihani yao.

Aidha, amewataka walimu na wazazi kushirikiana ili kuweza kubaini na kuwapata wazazi ambao wanawashawishi watoto wao kuandika majibu ya uongo katika mitihani yao ambapo pia amesema sheria ya elimu inakataza na inatoa adhabu kwa mtu yeyote anayemzuia mtoto kwenda shule.

Kwa upande wao maafisa elimu wa msingi na sekondari katika halmashauri ya Nanyamba wamesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafuatilia shule na walimu  ili wanafunzi wafanye vizuri katika masomo yao,  hii ikiwa ni kutokana na halmashauri hiyo kuwa nyuma kielimu.

Hata hivyo wadau wa elimu walioshiriki katika kikao hicho wametoa maoni yao katika suala hilo huku wakiitaka serikali kuingilia kati suala la elimu na kuboresha miundombinu ya elimu katika Halmashauri hiyo.





MANDA AAGIZA KUKAMATWA KWA WAZAZI WANAODAIWA KUWAFUNDISHA WATOTO KUJAZA MAJIBU YA UONGO. MANDA AAGIZA KUKAMATWA KWA WAZAZI WANAODAIWA KUWAFUNDISHA WATOTO KUJAZA MAJIBU YA UONGO. Reviewed by safina radio on February 15, 2018 Rating: 5

No comments